Ghasia zimekumba mji mkuu wa
Tanzania Dar es Salaam kufuatia
maandamano kuhusiana na kukamatwa
kwa kiongozi wa dini ya kiislamu
sheikh Ponda Isa Ponda. Waumini wa dini hiyo wamekabiliana na
polisi punde tu baada ya sala ya
ijumaa. Ghasia zilitokea katika mtaa wa
Simbazi eneo la Kariokor na kupelekea
maduka kufungwa huku watu
wakitawanyika kukimbilia usalama wao. Mwandishi wa BBC mjini humo Eric
David Nampesya alisema kuwa polisi
walitumia gesi ya kutoa machozi ili
kuwatawanya watu kadhaa waliokuwa
wamekusanyika wakitishia kuandamana
hadi katika eneo la Kidongo Chekundu kudai malalamiko kadha wa kadha. Kikosi cha jeshi la polisi kilishirikiana na
polisi mjini Dar Es Salam kukabiliana na
waandamanaji waliokuwa wamesema
watafanya maandamano baada ya
sala ya Ijumaa. Sheikh Ponda alikamatwa kwa madai
ya uchochezi. Kwingineko kisiwani Zanzibar polisi
walipambana na makundi ya vijana
waliokuwa wanataka kuachiliwa kwa
kiongozi wa kidini Farid Adi,
aliyetoweka siku ya Jumanne usiku.
Serikali imesema kuwa haijahusika kivyovyote na kutoweka kwa sheikh
Adi. Polisi walitumia gesi ya kutoa machozi
kutawanya makundi ya vijana
waliokuwa wanafanya vurugu. Afisa mmoja wa polisi aliuawa katika
ghasia zilizofanyika siku ya Jumatano
baada ya taarifa za kutoweka kwa
sheikh Adi kutolewa. Polisi
wamewakamata watu kadhaa
kuhusiana na vurugu hizo.